MJUE TENA MKWAWA SHUJAA

Faham  eneo alipozikwa Mkwawa eneo ambalo tarehe 4 Januari mwaka 1999 Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizindua Mara wa Kumbukumbu ya miaka 100 ya kifo cha Mkwawa (1898-1998) Mkwawa alikuwa mtoto wa Mtemi Munyigumba mama yake Mkwawa aliitwa Sengimba kutoka uzao wa mtemi wa Ilole mjukuu wa Sekindole. Mkwawa aliamua Kalenga ikiwa kando ya Mto Ruaha kuwa Makao Makuu ya Himaya yake yakiwa na Makazi Rasmi na Kituo cha Kijeshi Kwa mujibu wa kamanda wa Kijerumani Ernst Nigmann (mwaka 1920 alikuwa na cheo Kanali) katika kitabu chake “Die Wahehe” Mkwawa alitawala kutoka Uhehe akisaidiwa na watawala aliowateua wakiitwa Vangazila wakiwa na mamlaka yote ya utawala huku wakimfahamisha Mtemi Mkwawa taarifa muhimu wakikusanya watu katika vita na shughuli za kijamii, vijana waliofunzwa kwa ajili ya vita waliitwa Vigendo, washauri wa mtemi masuala ya kiutawala waliitwa Vitambule, wapelelezi waliitwa Vatandisi, kikosi maalum cha kuwasaka maadui waliotoroka kiliitwa Vandagandaga, kikosi cha mapigano kikiitwa Fipuka huku wapiganaji wakongwe wenye uzoefu wakiitwa Vatengelamtwa. Mkwawa alikuwa amepanua himaya yake upande wa kusini hadi Makamabako aliwashinda pia Wanyamwezi, Wagogo, Wamasai, Wasagara. na Wasangu moja ya mapigano ya kihistoria ni katika utawala wa Mkwawa ni yale ya mwaka 1882 alipopambana na Wangoni wakiongozwa na Chaburuma katika eneo la Makambako huku Wabena wakichangia mafanikio ya Mkwawa eneo la Itombolo kwa kujiunga na vikosi vya Mkwawa wakiitwa Vinamwani (Rejea G.M Culwick katika kitabu chake UBENA OF THE RIVERS na Nyagawa katka kitabu chake A HISTORY OF THE BENA TO 1914). Pia vikosi vya Mkwawa vilishambulia mara kwa mara misafara ya biashara kutoka Pwani kuelekea Bara kulikowalazimu Waarabu kujenga uhusiano wa kibiashara na Mkwawa kwa kusambaza nguo, bunduki na baruti huku wakibadilishana na pembe za ndovu na vipusa. Kwa mujibu wa Makumbusho ya Kalenga Mkwawa alikuwa na wake zaidi ya 62 hata hivyo ni wake 7 ndo walikuwa maarufu ambao ni Semsilangunda, Seluhwavi, Senyenza, Sechavala, Samwengamagoha, Senzalawahe, na Semelele. Wajerumani walipofika walikuta Mkwawa akitoza kodi misafara ya wafanyabiashara ilyopita uhehe, Mkwawa alijulikana kwa mbinu za kivita wana intelijensia wake walipanda kwenye miti mirefu kutoa taarifa za mwenendo wa adui taarifa zilimfikia haraka kwa watu kupokezana taarifa kwa kujipanga umbali unaofika kilometa nne kati ya mtu na mtu. Vikosi vya Mkwawa viliweza kufika Kisaki, Kilosa, Mpwapwa na Kilimatinde. Mara baada ya kusikia shughuli za Wajerumani maeneo ya Pwani Mkwawa alianza kujenga Ngome ya Kalenga mwaka 1887 ikijulikana kwa jina la Lipuli ikitokana na jina la Kinyamwezi ILPULI likimaanisha uimara wa Tembo. Mkwawa aliona umuhimu kwa watawala wenyeji kuungana ili kuwashinda Wajerumani. Mkwawa aliwatumia ujumbe Mtemi Isike wa Tabora na Chabruruma wa Ungoni ili waungane kupambana na Wajerumani hata hivyo walikataa, baada ya wajumbe waliotumwa kupeleka ujumbe wa amani kuuwawa Februari 1891 Mkwawa aliamuru vikosi vyake kushambulia ambavyo viliweza kufika na kushambulia ngome ya Kilosa huku walinzi wa kituo cha kijeshi wakiuwawa pia aliagiza kufungwa kwa njia za biashara ya masafa marefu kutoka Pwani kuelekea Tabora zilizopita katika himaya yake jambo ambalo liliwakera Wajerumani. Katika kukabiliana na tishio la Mkwawa Wajerumani walijenga ngome za kijeshi kakika maeneo ya Mahenge na Kisaki (Rejea G C K Gwassa Katika The German intervention and African resistance in Tanzania). Mkwawa alikataa kutembelea Dar es salaam baada ya kuitwa na Wissmann kiongozi wa wakati huo hata hivyo alipeleka ujumbe Mpwapwa kuonana na Wajerumani ambao ulipokelewa ingawa Machi 1891 Herman Von Wissmann (1888-1891) aliachishwa kazi kutokana na matumizi makubwa ya uendeshaji akitumia Pauni za Kiingereza laki nne na nusu (£450,000) badala ya pauni Laki Moja zilizoidhinishwa (£100,000), mwanadiplomasia Julius Von Sedon akateuliwa kuwa Gavana, (Rejea John Iliffe katika kitabu chake - A Modern History of Tanganyika). Tarehe 17 Agosti 1891 Wajerumani wakiwa katika kombania tatu wakiongozwa na Emil von Zelewski akisaidiwa na maluteni wawili Wilhelm na Egon walipiga kambi Ilula wakiwa njiani kuelekea Kalenga walipofika Lugalo waliangamizwa na vikosi vya Mkwawa vikiongozwa na Mpangile ndugu yake Mkwawa, mwaka 1892 yalitokea mapigano ya Munisigara karibu na ngome ya Wajerumani ya Kisaki. Kutokana na ujasiri na uwezo ulioonyeshwa na Vikosi vya Mkwawa Gavana Fredrick Von Schele aliamua kumuita Tom Von Prince (Bwana Sakarani) aliyesifika kwa ukatili wake kuwa kamanda wa Ngome ya Iringa baada ya kuwa ameongoza kwa mafanikio mapigano na kumshinda mtemi Isike wa Tabora mwaka 1893. Fredrick Von Schele alitumia muda mwingi kufuatilia mbinu za mapigano zilizokuwa zkitumwa na Wahehe. Kambi ya Kijeshi ilianzia Miyomboni Iringa watu wa kwanza kuishi walikuwa Askaris (Askari) wakiwa ni wapiganaji wa Kiafrika kutoka jamii mbalimbali wakiweka makazi na familia zao katika eneo ambalo sasa ni Kituo kikuu cha Polisi. Wajerumani wakiamini wamejiimarisha Kijeshi vya kutosha Fredrick Von Schele akiwa msimamizi wa jumla huku vikosi vikiongozwa na Tom Von Prince (Bwana Sakarani) vikitokea Tosamanganga vikisaidiwa na watawala wa jadi waliopigana upande wa Wajerumani akiwemo mtemi Merere wa Usangu ambaye alikubali kupigana upande wa Wajerumani walivunja ngome ya Mkwawa huko Kalenga na kumshinda Mkwawa tarehe 30 Oktoba 1894, Gavana akiwa Fredrick Von Schele (1893-1895). Mkwawa aliendelea kupambana na Wajerumani akiwa mafichoni, Gavana aliyefuata Eduard von Liebert (1896-1901) akitoa zawadi ya Rupia 5,000 kwa atakayewezesha kupatikama kwa Mkwawa kwa miaka mine hakuna aliyeweza kumkamata Mkwawa hadi tarehe 19 julai 1898 Mkwawa alijiua baada ya kuzingirwa na Wajerumani wakiongozwa na sajini Merkl. Kwa mujibu wa Jumba la Makumbusho la Mkoa wa Iringa kosa alilifanya Mkwawa ni kurudi usiku kuangalia iliyokuwa Ngome yake ya Kalenga kulikosababisha Wajerumani kumfuatilia. Wajerumani walikata kichwa cha Mkwawa na kukipeleka Ujerumani huku mwili wake ukizikwa Mwambalasi.

Comments

Popular posts from this blog

FAIDA ZA VITAMIN C MWILINI

VYAKULA NA MATUNDA VINAVYOONGEZA NGUVU ZA KIUME

MATATIZO SUGU YA KOMPYUTA ,MBINU ZA KUONDOA TATIZO